Jumapili 8 Novemba 2026 - 21:48
Chama cha Democrats na Republicans Havuna Tofauti Katika Uadui Dhidi ya Mataifa ya Kanda

Hawza/ Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Chama cha Hizbullah nchini Lebanon, Sheikh Ali Da'moush, amesisitiza kuwa; mabadiliko ya vyama vya kisiasa nchini Marekani na ushindi wa Democrats hayawezi kuathiri sera za uhasama za nchi hiyo wala kuacha kuunga mkono utawala wa Kizayuni.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Da'moush, Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Hizbullah nchini Lebanon, amesema hayo katika khutuba ya Swala ya Ijumaa iliyofanyika katika jengo la kidini la Sayyidah Zaynab (a.s), lililopo Bir al-Abed.

Akizungumza katika khutuba hiyo, alionya kuhusu uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Lebanon na mashinikizo ya Washington yanayolenga kuiondolea silaha Muqawama. Alisisitiza kuwa Muqawama, kwa kutegemea utamaduni wa Ashura, hautasalimu amri mbele ya mashinikizo hayo. Aidha, aliitaka serikali ya Lebanon kuchukua msimamo wa kitaifa na wa dharura katika kuilinda na kuitetea sehemu ya kusini mwa nchi hiyo.

Kutokuwepo tofauti kati ya Democrats na Republicans katika sera za uhasama

Sheikh Ali Da'moush, akizungumzia mabadiliko ya kisiasa nchini Marekani, alisisitiza kuwa; kushindwa kwa Donald Trump na chama cha Republicans katika uchaguzi wa katikati ya muhula pamoja na ushindi wa chama cha Democrats hakutabadilisha malengo ya uhasama wa Marekani dhidi ya mataifa ya eneo hili.

Aliongeza kuwa; malengo ya serikali za Marekani zinazofuatana katika eneo hili yako wazi, nayo ni kutawala eneo hili na nchi zetu pamoja na kuunga mkono utawala wa Kizayuni.

Alieleza kuwa; serikali hizo zimekuwa zikifanya juhudi za kutimiza malengo yao ya kudumu, ambayo hayana tofauti baina ya serikali moja na nyingine, rais mmoja na mwingine, wala baina ya mwanachama wa Republicans na wa Democrats. Tofauti pekee inayoweza kujitokeza ni katika mbinu wanazotumia.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hizbullah alibainisha kuwa, ingawa kushindwa kwa Trump katika uchaguzi wa katikati ya muhula kulitokana na vita dhidi ya Iran, kushindwa kwake katika medani hiyo, pamoja na kuongezeka mabadiliko katika mitazamo ya wananchi wa Marekani kuhusu utawala wa Kizayuni na suala la Palestina, jambo hilo halimaanishi kuwa sera za Marekani kuhusu «Israel» zimebadilika. Alisisitiza kuwa yeyote anayefikiri ushindi wa Democrats utaleta mabadiliko katika mwelekeo huo wa Marekani amekosea.

Upinzani mkali dhidi ya uingiliaji wa Marekani na mpango wake wa kuchochea fitina nchini Lebanon

Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Hizbullah, akizungumzia hali ya ndani ya Lebanon, alisema: «Jambo muhimu kwetu nchini Lebanon ni kuizuia Marekani kuingilia masuala ya ndani ya nchi yetu na kukomesha utawala wake wa kimabavu dhidi ya nchi hii. Hii ni kwa sababu uingiliaji wa Marekani umefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Nchi hiyo inalazimisha matakwa yake katika maamuzi ya kisiasa, kiusalama, kimahakama na kifedha, na kuwachochea wananchi wa Lebanon wagombane wao kwa wao».

Aliongeza kuwa mpango wao ni kuzusha fitina na mifarakano miongoni mwa Walebanon, jambo ambalo hawataruhusu kamwe litekelezwe, na watakabiliana nalo kama walivyofanya huko nyuma.

Aidha, alisema Marekani inaendelea kuweka mashinikizo kwa lengo la kuuondolea silaha Muqawama, wakati huohuo ikiupa utawala wa «Israel», ambao ni muuaji na mvamizi wa ardhi za wengine, uhuru wa kushambulia na kuharibu kwa mauaji, uharibifu na milipuko vijiji vya kusini mwa Lebanon. Vilevile, Marekani inatoa mwavuli wa kisiasa kupitia «makubaliano ya mfumo» ili kuhalalisha uvamizi na uchokozi huo.

Marekani ndiyo chanzo kikuu cha majanga yote, na lengo lake ni kuitawala Lebanon na kuuvua silaha Muqawama

Sheikh Da'moush alisisitiza kuwa; Marekani haifikirii kamwe kuhusu maslahi ya Lebanon, bali ndiyo chanzo kikuu cha majanga yote yanayoikumba Lebanon, eneo hili na dunia nzima. Aliongeza kuwa Marekani itaendelea kuiwekea mamlaka ya Lebanon mashinikizo ili kujipatia manufaa na masharti zaidi. Alifafanua kuwa: «Hatutakubali kushindwa na mashinikizo yoyote.

Pamoja na wananchi wetu, tutatumia haki yetu ya wazi na ya kimaumbile ya kufanya Muqawama na kulinda ardhi yetu». Aidha, aliiomba serikali ya Lebanon ichukue msimamo unaolingana na uzito wa hatua hii na hadhi ya wananchi wake, na ishughulikie suala la kusini mwa Lebanon bila kuzingatia hesabu za kisiasa wala maagizo ya Marekani na Wazayuni.

Sheikh Da'moush aliongeza kuwa; haikubaliki kwa serikali kuchukua sera ya kutojali mbele ya uharibifu na mashambulizi yanayoendelea kusini mwa Lebanon, kana kwamba eneo hilo si sehemu ya Lebanon. Alisisitiza kuwa kusini mwa Lebanon kwa sasa si mkoa tu wa nchi hiyo, bali ni «Lebanon nzima».

Alifafanua kuwa serikali yoyote inayowaheshimu wananchi wake na mamlaka yake ya kitaifa inapaswa kulichukulia suala la kusini mwa Lebanon kama jambo la dharura la kitaifa, kiasi cha kusimamisha miradi mingine yote na kulipa kipaumbele suala la kusitisha mashambulizi, kukomesha uvamizi, kuwawezesha wakimbizi kurejea makwao, kujenga upya maeneo yaliyoharibiwa na kuitetea ardhi ya nchi hiyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha